The United Republic of Tanzania | Ministry of Information, Communication and Information Technology | ICT Commission
 INFORMATION AND COMMUNICATION TECHNOLOGY COMMISSION


Media Centre

Speech


Hounorable Jerry William Slaa (M.P) - Minister of Information Communication and Technology

Mheshimiwa Mhandisi Mary Prisca Mahundi, Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bwana Muhammed Hamis Abdula, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na timu ya Menejimenti iliyoko hapa. Profesa Leonard Msele, Mwenyekiti wa Bodi ya Tume yetu ya TEHAMA, pamoja na wajumbe wa Bodi mlioko hapa. Dr. Nkundwe Mosses Mwasaga, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA na menejimenti yako mlioko hapa. Waheshimiwa mabalozi wanaoziwakilisha nchi mbalimbali hapa nchini, natambua uwepo wa Balozi anayewakilisha Jumuiya ya Ulaya, Mheshimiwa Balozi wa Finland, Italia, Mwakilishi Mkazi wa UNESCO, Bwana Michael Toto, Dr. Greek Dawn ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Huawei Tanzania, na ndiye Mdhamini wetu mkuu kwa siku ya leo. Wakuu wa Taasisi za Serikali na sekta binafsi mlioko hapa, Wakurugenzi Wakuu wa Taasisi za Umma mlioko hapa, wadhamini wetu, washiriki wa kongamano kutoka sekta za umma na binafsi, na wale wanaotufuatilia kupitia matangazo ya moja kwa moja. Wageni waalikwa, waandishi wa habari, mabibi na mabwana, nawasalimu kwa jina la Muungano wa Tanzania… kazi iendelee!

Ndugu washiriki, kwanza kabisa napenda kumshukuru Mungu kwa kutukutanisha siku ya leo tukiwa na afya njema, na kutuwezesha kushiriki katika Kongamano la Nane la TEHAMA. Pili, namshukuru na kumpongeza Bwana Muhammed Hamis Abdula, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na kamati nzima ya maandalizi ya kongamano hili - hongereni sana!

Pia kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya wana TEHAMA kutoka sekta ya umma na binafsi, niseme nimefarijika sana kuwa sehemu ya Jumuiya hii, ambayo pia mimi ni sehemu yake. Nilikuwa naangalia huku kwenye hadhara na nikajiuliza jinsi nitakavyoweza kuwa sehemu ya jumuiya hii. Nimemuona mwanafunzi mwenzangu Tatu Mikdadi, na nadhani kuna wengine pia wako katika sekta mbalimbali, nawashukuru sana!

Ndugu washiriki, ninawashukuru wadhamini na wadau wote wa maendeleo ya miundombinu ya TEHAMA, ubunifu katika TEHAMA, kuendeleza ujuzi na ubunifu katika TEHAMA, watafiti katika TEHAMA, wawekezaji na wadau wote kwa uwepo wenu hapa na kufanikisha shughuli hii muhimu kwa leo.

Nichukue nafasi hii kuwapongeza mabalozi wanaoziwakilisha nchi mbalimbali na washiriki wa kimataifa ambao mmeona umuhimu wa kutenga muda wenu ili kuhakikisha kongamano hili la nane linafanikiwa. Karibuni sana! Nategemea kuwaona katika makongamano mengine yajayo!

Ndugu washiriki, wizara ninayoiongoza, pamoja na majukumu mengine, imepewa jukumu la kusimamia Sera ya TEHAMA ya mwaka 2016, ambayo imeainisha masuala ya kisera, kisheria, na taasisi katika kukuza sekta ya TEHAMA nchini. Katika kutekeleza sera ya TEHAMA, Serikali kupitia amri ya Rais, iliunda Tume ya TEHAMA ambayo ilipewa majukumu yafuatayo:

       Kusimamia utekelezaji wa Sera ya TEHAMA.

       Kukuza uwekezaji katika sekta ya TEHAMA.

       Kujenga uwezo na kukuza utaalamu katika fani ya TEHAMA.

       Kushirikiana na wadau wengine katika masuala ya utafiti.

Ndugu washiriki, utekelezaji wa majukumu haya ndio umesababisha kuwepo kwa kongamano hili, ambapo wadau na wataalamu mbalimbali wanapata nafasi ya kujadili masuala mbalimbali yatakayowezesha utekelezaji wa Sera ya TEHAMA nchini, lakini pia kuweka mikakati ya kwenda sawa na mabadiliko ya kiteknolojia yanayoibuka, hasa katika nyanja za akili bandia, roboti na uchambuzi wa takwimu kubwa (Big Data Analytics).

Ndugu washiriki, nimejulishwa kuwa kongamano hili ni la nane tangu kuanzishwa kwa Tume ya TEHAMA. Pia nimejulishwa kuwa kongamano hili limetanguliwa na mkutano wa wanawake wanaoshiriki katika TEHAMA pamoja na vijana wanaojihusisha na TEHAMA, ambapo masuala mbalimbali kuhusu maendeleo ya TEHAMA yalijadiliwa.

Leo hii nitafungua kongamano hili ambalo lina kaulimbiu isemayo "Kutumia Uwezo wa Akili Mnemba na Roboti kwa Mapinduzi ya Kijamii na Kiuchumi." Kaulimbiu hii inafungua mjadala muhimu sana, kwa wakati huu ambapo dunia nzima inashuhudia mapinduzi ya kidijitali.

Sisi kama taifa tunayo nafasi ya kutumia teknolojia hizi ili kuboresha ustawi wa wananchi wetu na kuongeza tija katika uchumi. Ndugu washiriki, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoongozwa na Mheshimiwa Dr. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeendelea kupiga hatua kubwa katika TEHAMA, ambayo ni nguzo kuu ya kufikia uchumi wa kidijitali - yaani, Digital Economy.

Dunia hivi sasa ipo katika mapinduzi ya nne, tano na sita ya viwanda, yaani Mapinduzi ya 4th, 5th, na 6th Industrial Revolution, ambapo shughuli za kiuchumi, kijamii na uzalishaji kwa kiasi kikubwa zinakwenda kuendeshwa kwa kutumia teknolojia za juu za TEHAMA.

Kwa umuhimu huo, serikali imeendelea kuwekeza katika kufanya maboresho ya kisera, kisheria na kitaasisi pamoja na kujenga uwezo kwa Watanzania ili kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa sehemu ya mabadiliko katika masuala ya TEHAMA duniani.

Ndugu washiriki, tumeshuhudia namna ambavyo akili mnemba na roboti zina uwezo wa kuboresha huduma za kijamii na kukuza uchumi wetu kwa njia ambazo zilikuwa hazifikiriki miaka michache iliyopita. Nimetembelea mabanda mbalimbali na kujionea namna ambavyo teknolojia ya akili mnemba na roboti inaweza kutumika katika sekta mbalimbali kama vile afya, ambapo akili mnemba na roboti vinaweza kusaidia kutoa utambuzi wa haraka wa magonjwa na kuboresha huduma za afya msingi.

Katika sekta ya kilimo, akili mnemba na roboti zinaweza kuboresha tija kwa wakulima kwa kusaidia katika usimamizi bora wa uzalishaji na utafiti wa hali ya hewa. Pia teknolojia hii inaweza kubadilisha kabisa jinsi tunavyoendesha biashara na utengenezaji wa bidhaa kwa kuboresha mifumo ya usambazaji na kuongeza ufanisi.

Kwa kutumia akili mnemba na roboti, viwanda vyetu vinaweza kuongeza uzalishaji na kuwa na ushindani katika soko la kimataifa. Aidha, akili mnemba na roboti zinaweza kuimarisha mifumo ya elimu kwa kusaidia upatikanaji wa elimu bora kwa kila mwanafunzi bila kujali eneo au hali yake ya kiuchumi. Kwa njia hii, tunaweza kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata fursa ya kujifunza na kuchangia katika maendeleo ya taifa letu.

Ni matumaini yangu kuwa kongamano hili litawezesha kujifunza zaidi na kupata uzoefu katika matumizi sahihi ya akili mnemba na roboti ili kuboresha utendaji kazi na utoaji huduma katika maeneo yetu.

Ndugu washiriki, nimejulishwa kuwa katika kongamano hili kulikuwa na maonyesho ya roboti kutoka kwa wanafunzi wa sekondari ambao wameonyesha ubunifu mkubwa na uwezo wa hali ya juu katika teknolojia. Nimejulishwa pia kuwa wanafunzi hao hawakutoka tu kwenye shule za mchepuo wa Kiingereza, lakini pia mchepuo wa Kiswahili kama vile shule za Azania, Jangwani, na Tambaza.

Kitendo hiki cha wanafunzi kutoka shule mbalimbali kuonyesha ubunifu wao kimeonyesha ukuaji wa teknolojia na uwezo wa kidijitali nchini. Inaonyesha kuwa shule zote na wanafunzi wa shule zote wana uwezo wa kuonyesha vipaji vyao katika ubunifu. Ninawaelekeza ICTC kuwasaidia kuwalea, lakini pia kuwasimamia wanapojiandaa kuelekea mashindano yatakayofanyika nchini Uturuki ili uwezo wao uweze kuonekana na kuleta matokeo bora na ushindi kwa Taifa letu.

Tanzania, kama ilivyo kwa nchi zingine zinazoendelea, inakabiliwa na changamoto hasa kwenye jamii zetu ambazo zinahitaji suluhisho la haraka na endelevu. Teknolojia za akili mnemba na roboti zinaweza kutusaidia kutatua changamoto hizi kwa kuongeza ufanisi, kupunguza gharama, na kuleta ubunifu katika sekta mbalimbali kama nilivyosema hapo awali: sekta ya afya, kilimo, elimu, na usimamizi wa rasilimali.

Kwa hiyo, kongamano hili ni fursa ya kutafakari na kujadili hatua za kuchukua ili kuhakikisha kuwa teknolojia hizi zinatumiwa vyema kwa manufaa ya Taifa bila kuathiri masuala ya kiuchumi, kiusalama na tamaduni zetu.

Ndugu washiriki, ni matarajio yangu kuwa baada ya kongamano hili tutapata taarifa inayojumuisha maono yenu kuhusu maendeleo ya TEHAMA, pamoja na mapendekezo ya namna ya kuboresha sera na sheria zetu za kisekta ili kuweza kuchochea ukuaji na matumizi ya TEHAMA katika kuchangia pato la Taifa na kutoa huduma kwa wananchi.

Ndugu washiriki, baada ya kusema hayo, natangaza rasmi sasa kwamba Kongamano la Nane la TEHAMA kwa mwaka 2024 limefunguliwa rasmi!

Asanteni sana kwa kunisikiliza!

11036A9928