Media Centre
Speech
Dar es Salaam Oye, Dar es Salaam Oye!
Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Waziri wetu na Wizara yake, pamoja na Wageni wetu wote waalikwa, Mabibi na Mabwana. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania!
Kazi Iendelee!
Mheshimiwa Waziri Mkuu, nashukuru kwa kuchagua Dar es Salaam kuwa mwenyeji wa tukio hili. Nimeona kaulimbiu kuu ya mwaka huu, ambayo imenipeleka mbali, na kwa kifupi, nasema hivi: Masuala ya Artificial Intelligence, kwa lugha nyepesi ni kama kuiwezesha kompyuta au mashine kufikiri, kuelewa, na kutenda kama binadamu. Kwa kufanya hivyo, taaluma ya falsafa ina matawi yake, na tawi la kwanza linaitwa axiology, ambalo linafuatilia chimbuko na mabadiliko ya jambo. Matawi mengine ni mantiki (logic), epistemology, metaphysics, falsafa ya kisiasa, maadili (ethics) na mengine mengi.
Moja ya mambo muhimu kuhusu artificial intelligence ni uwezo wa kuzipa mashine uwezo wa kufikiri, na katika taaluma ya falsafa, kufikiri kunaangukia kwenye mantiki. Ikiwa mashine zitapata uwezo wa kufanya kazi kama binadamu, basi uwezo wa binadamu utakaribia kuwa sawa na kile anachokivumbua.
Hii ina maana kwamba msingi mkubwa wa artificial intelligence unaanzia kwa binadamu mwenye uwezo wa kufikiri kwa ufasaha, kugundua na kuvumbua, ili mwisho wa siku tuweze kupata sayansi inayolingana na anavyoweza kufikiria.
Nashukuru kwa kile tulichojifunza hapa, mambo makubwa na muhimu. Jambo moja kubwa ambalo nimeona ni kwamba kongamano hili limeendeshwa kwa Kiswahili. Tukiendelea kutumia Kiswahili, watu wengi wataendelea kuelewa na kuwa na uwezo wa kuwasilisha kile tulichojifunza. Hii ni kwa sababu tunaumiliki na ustadi wa Kiswahili hapa Tanzania, na hilo linatusaidia kupata maarifa, ujuzi, na kuwasiliana kwa urahisi kuhusu mada muhimu kama hii.
Nawakaribisha tena mkoani Dar es Salaam, na ninawahakikishia mkoa wetu ni salama kwa yeyote kuishi hapa. Wageni ambao mmetoka mbali, Dar es Salaam ni jiji kubwa sana, lenye idadi ya watu takriban milioni 5.3 kwa mujibu wa sensa ya mwaka jana. Mkiwa na muda, nawaalika kutembea na kufurahia vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo hapa. Nina hakika kwamba mtavutiwa na tutafanya kila jitihada kuhakikisha mnaondoka na furaha mliyokuja nayo.
Asanteni sana!